WASOMI WA UFINI KUZURU MAABARA YA C4D FEBRUARI

Kundi la wanafunzi kutoka chuo kikuu cha Aalto kinachopatikana nchini Ufini, wataizuru maabara ya technolojia ya C4DLab inayopatikana katika bewa la Sayansi Asilia na Viumbe, Ndaki ya Nairobi.

Wanafunzi hao sita ni miongoni mwa wanafunzi wengine ishirini wanaoendeleza masomo yao kwa mpango wa uvumbuzi katika maabara hiyo na watapata nafasi kujiunga na wenzao katika semina ya siku mbili. Baadaye, wavumbuzi hao, ambao ni jumla ya watu ishirini na sita wataelekea nyanjani ili kukusanya data kuhusiana na matatizo wanayoyatatua katika jamii.

Mpango wa uvumbuzi katika maabara ya C4DLab ulianzishwa na mkurugenzi wa maabara hiyo Bw. Tonny Omwansa ili kuwaandaa wanafunzi kwa maisha ya kesho na kuwashirikisha katika utafiti na uvinjari wa vikwazo katika jamii na kubuni suluhisho mwafaka.

Picha ya kikundi cha Wavumbuzi wa mwaka 2019/2020

Mpango huo ulianzishwa mwaka wa 2017 na hukumbatia mchakato wa mawazo ya kubuni, almaarufu, Design Thinking Process kuafikia malengo yake. Wanafunzi wanaosajiliwa katika mpango huo hushiriki mafunzo na kuwekwa katika timu mbalimbali huku wakitarajiwa kushirikiana katika timu hizo ili kusuluhisha shida ibuka katika jamii.

Ikumbukwe kwamba, wanafunzi wanaounda timu hizo wanaustadi katika nyanja tofauti tofauti hivyo basi huwekwa pamoja ili kusaidiana kimawazo na kimtazamo.

Wanafunzi hao sita watakuwa nchini kwa muda wa wiki mbili kabla ya kurejea Ufini kuendeleza mradi huo. Wasomi wa humu nchini watasaidia kupanga mkutano wa kilele wa Masomo yanayolenga matatizo katika jamii, almaarufu Problem Based Learning (PBL) katika bara Afrika, mkutano ambao utaandaliwa katika chuo kikuu cha Nairobi mwezi Juni mwakani.

Mwaka huu, wanafunzi watatu katika mpango huo wa uvumbuzi, wataandamana pamoja na mshauri wao mmoja kuelekea Afrika kusini ili kushiriki katika koongamano linaloafiki lengo la kuimarisha mfumo wa ikolojia ya uvumbuzi nchini na barani Afrika, haswa miongoni mwa vijana.

2 Comments to “WASOMI WA UFINI KUZURU MAABARA YA C4D FEBRUARI”

Leave A Comment